Waziri wa mifugo na Uvuvi mhe. Mashimba Ndaki amesema serikali ya Tanzania bado inalitambua soko kuu la kimataifa la Kasenda kuwa ni miongoni mwa masoko matatu ya kimataifa ambayo yanatumika kutoa vibali ili kuhakikisha mazao ya samaki yanayopelekwa katika mataifa mengine yanakuwa katika ubora wa hali ya juu.
Waziri Ndaki ameyasema hayo leo tarehe 13.12.2021 wakati wa ziara yake ya kuongea na wananchi na wafanya biashara katika soko la kimataifa la Kasenda lililopo kata ya Muganza wilayani hapa.
"Tanzania tuna masoko matatu tu ya kimataifa, soko la samaki la Feri lililopo Dar es Salaam, Soko la Kirumba lilolopo jijini Mwanza na Kasenda lililopo Chato. Nataka niwahakikishie soko lenu la Kasenda lipo pale pale na lipo kimkakati chini ya Wizara ya Mifugo na uvuvi, halikuletwa hapa kwa bahati mbaya" alisema mhe. Waziri Ndaki.
Waziri Ndaki amesema masoko mengine yanayotajwa na baadhi ya watu hayapo na Wizara haiyatambui kwani masoko hayo matatu yanalindwa na miongozo pamoja na mindombinu ambayo serikali imewekeza katika masoko hayo.
Waziri Ndaki amesema kwa mwaka 2020/2021serikali kupitia Wizara imeweza kukusanya mapato ya zaidi ya shilingi bilioni mbili kutoka katika soko la Kasenda
"kwenye soko hili tumewekeza fedha nyingi, tunao watumishi pia wa Wizara hapa zaidi ya watano kwa hiyo lazima tulilinde" alisisisitiza Mhe. Waziri Ndaki.
Aidha Waziri Ndaki ameonya tabia ya baadhi ya viongozi kuwabughuzi wafanya biashara kwa kuwataka wakate leseni za uvuvi katika maeneo wanayofanyia shughuli za uvuvi hivyo amesema wafanya biashara watatumia leseni zao bila kujali leseni imekatwa wapi, "sasa hivi hata ukikata leseni ya uvuvi ukiwa mkoa wa Mara unaweza ukafanya shughuli za uvuvi hata ukiwa Chato, hakuna tatizo kabisa..kuwalazimisha wafanyabiashara kukata leseni za uvuvi kila wilaya kitendo hiki ni kinyume na sheria zetu na kufanya hivyo ni kinyume na sheria" alisistiza Waziri Ndaki.
Mapema akimkaribisha Waziri Ndaki Mbunge wa jimbo la Chato mhe.Medard Kalemani amesema wafanyabishara wa dagaa wanaotumia soko la Kasenda kwa sasa wameathirika sana kutokana na kauli za baadhi ya viongozi kuwazuia wafanyabiashara hao kupitishia mizigo yao kwenye soko la Kasenda ambapo amesema kutokana na madhara hayo hivi sasa soko hilo linao wafanyabishara 10 tu waliobaki katika soko hilo ambapo hapo awali zaidi ya watu 13,000 walinufaika na soko hilo.
Mhe. Kalemani pia amesema hapo awali soko hilo liliweza kuingiza mapato kiasi cha shilingi milioni 14 kwa siku lakini hivi sasa mapato yanaishia shilingi laki 8 kwa siku ambapo zaidi ya tani 30 za dagaa ziliipitia katika soko hilo lakini kwa sasa dagaa dagaa wamepungua sana.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chato mhe. Bathromew Manunga amesema soko la Kasenda kwa sasa kumekuwa likiingiliwa na kauli za baadhi ya viongozi kutoka Wilaya jirani ambazo zinawachanganya wafanyabishara na kusababisha baadhi ya wananchi wa Kasenda kutaka kujichukulia sheria mkononi kwa kukasirishwa na kauli za viongozi kutoka Wilaya jirani juu ya matumizi ya soko hilo la Kasenda.
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.