Mkuu wa wilaya ya Chato Mhe. Said Nkumba April 16, 2024 aliongoza mamia ya wananchi kijiji cha Igando kata ya Bwera pamoja na wananchi wa kata ya Bukome wilayani hapa kushiriki zoezi la uchimbaji wa misingi ya miradi minne ya kuondoa umaskini yaani TASAF, OPEC awamu ya iv yenye thamani ya zaidi ya milioni mia nne.
Nkumba amekiri kufurahishwa na wananchi hao jinsi walivyoonesha kiu ya maendeleo kwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi hilo ambapo amewasihi waendelee na moyo huo huku akiwataka mafundi kukamilisha ujenzi ndani ya muda wa mkataba kwani kwa kufanya hivyo wanaishawishi Serikali kuwapelekea miradi mingine, huku akiwasisitiza wanavyojitolea kazi za maendeleo pia wajitoe kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni ili kuinua ufaulu pia kuepuka udumavu.
"Ukiona wananchi wanajitokeza kwa wingi kushiriki shughuli za maendeleo ujue viongozi wa eneo hilo wana mshikamano mkubwa hivyo hongereni sana, nawasihi kuwa viongozi sio mashati kwahiyo kama wanafanya kazi vizuri hakuna haja ya kuwabadilisha, binafsi namshukuru Rais wetu Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa anayoifanya kutuletea fedha za miradi, nawapongeza viongozi kuanzia Wenyeviti,Madiwani pamoja na Mhe.Mbunge wetu Kalemani kutupambania kuomba miradi hii na kweli inatufikia.Alisema Nkumba
Naye Mratibu wa TASAF wilaya ya Chato Bi Aisha Kesowani alitaja jumla ya fedha zilizopokelewa kiasi cha Tshs - 415,496,190.73 kwa mchanganuo wa; Jengo la wagonjwa wa nje (OPD)Tshs - 92,410,714.29 na Nyumba ya watumishi wa afya 2 in 1 Tshs - 92,410,714.29 ni miradi ya kijiji cha Igando kata ya Bwera, ambapo miradi ya kata ya Bukome ni Bweni la wavulana shule ya Sekondari Mkungo Tshs - 138,264.047.86 na nyumba ya walimu 2 in 1 Tshs - 92,410,714.29.
Aidha Bi Aisha alisisitiza kuwa miradi hiyo iliibuliwa na kuidhinishwa na wananchi wa maeneo hayo mnamo Septemba 2023 kupitia mikutano ya hadhara kwa kuangalia vipaumbele vya uhitaji katika maeneo yao, na kwa asili ya mradi ni jamii itachangia nguvu kazi kama kuchimba msingi, kujaza kifusi,maji ya ujenzi, mawe,mchanga,ulinzi wa vifaa vya ujenzi pamoja na kupanda miti ya matunda na kivuli
MKURUGENZI MTENDAJI
Postal Address: 116 CHATO
Telephone: +255282228007
Mobile:
Barua pepe: ded@chatodc.go.tz
Copyright©2016 CDC . All rights reserved.